Wednesday, September 8, 2010

Maamuzi juu ya Elimu yasiachiwe Mangimeza tu

TUMEONA huko nyuma jinsi wizara husika ilivyofikia maamuzi ambayo baadaye yamekuja kututokea puani na hasara zake zinaendelea mpaka leo.

Mojawapo ya hasara kubwa ambayo nchi hii inatarajiwa kuipata ni ile ya kuwa na kizazi cha wanafunzi wanaosoma na kuelewa njia moja katika kila somo kwa sababu ya udikteta wa wizara kuamua kuanzia sasa wanafunzi katika shule za umma Tanzania watakuwa wakitumia kitabu kimoja tu.

Hii ni sawa kabisa na kuonea kizazi husika kwa kuwanyima uhuru wa kuchagua na kujifunza kutoka vyanzo mbalimbali. Nalo jambo hili linafanyika wakati ambapo tayari vitu kama intaneti vina maelfu ya vitabu juu ya kila somo lililopo ulimwenguni kwa lugha nyingi tu hapa duniani.

Ni kwa sababu hii ndio maana kwa kuangalia nyuma pale waziri mmoja wa elimu alipostopisha michezo mashuleni kwa sababu eti ndiyo inayochangia wanafunzi kufeli tumeonelea tutoe wito kwa wakerketwa wa elimu na maendeleo ya wanafunzi, shule na vyuo kuanza kampeni ya kukataa kabisa kukubali maamuzi yanayofanywa na mangimeza katika wizara husika wengi wao watoto wao wakiwa hawasomi hapa Tanzania.

Tunaamini wawakiishi wa shule na vyuo mbalimbali ndio wanaostahili kuwa na mkutano wa kila mwaka kufanya maamuzi makubwa yanayohusu sekta hii na sio maamuzi hayo kufanywa na mangi meza wachache.

Elimu ni sekta ya ubia kati ya wazazi, wanafunzi, walimu na viongozi na wanajamii kwa ujumla. Ikiwa kama upande mmoja utapora jukumu la kufanya maamuzi juu ya welekeo na mtazamo stahilivu basi uamuzi huo ukiwa na matatizo unakuwa na hasara hata kwa wale ambao walijua toka mwanzo kuwa uamuzi husika una walakini.

Mathalani, katika uamuzi wa kusimamisha michezo mashuleni upo ushahidi tosha kuwa jambo hilo lilifanyika kinyemela na kwa utashi wa mtu binafsi. Katika miaka hii ambayo wazazi wanatambua fika kuwa baadhi ya watoto hao hawana 'akili' ya darasani lakini wana akili au vipaji katika michezo na sanaa lau kama wangeshirikishwa uamuzi huu usingepita bila kupingwa na pengine ungelitupiliwa mbali.

Faida za kuwashirikisha watu katika maamuzi yanayohusu masuala ya maendeleo ya elimu ni pamoja na:
. kuwa na mchakato wa kina na wa kitaalamu na wenye kuhabarishwa zaidi kabla maamuzi hayajafikiwa;
. pande zote kuchangia ubora au udhaifu wa hoja kwa namna ambayo huweza kuibua fikra mpya;
. maamuzi ya pamoja yanajenga umoja na mshikamano katika taasisi;
. maamuzi ya pamoja yanasaidia oganaizesheni kuwa na kumbukumbu ya maamuzi yote ya nyuma na hivyo kutokuwepo na hatari ya watu kurudia jambo ambalo lilikwishafanyika huko siku za nyuma.
. maamuzi ya pamoja huwafungisha mikono waamuzi wote na hivyo kutokuwa na kuwalaumu wengine endapo uamuzi huo ulikuwa mbovu au usiofaa kutokana na muktadha uliopo wakati huo.

Kwa maelezo hayo hapo juu ni dhahiri basi kuwa ni jambo zuri kila mara kuwa na mfumo shirikishi katika maamuzi yanayohusu maendeleo ya elimu, shule na vyuo kwa sababu ya kuepuka makosa na matatizo yanayoweza kuzushwa kutokana na maamuzi ya mtu mmoja na ya kidikteta.

Kiundeshaji lazima shule na vyuo viwe na bodi zake, menejimenti na mabaraza au kamati mbalimbali za ushauri. Maamuzi yote muhimu kuhusu sekta ya elimu ni lazima yajadiliwe kinagaubaga katika ngazi hizi kabla ya kujadiliwa katika ngazi za juu iwe tunafuata ujamaa au ubepari, tuwe nchi ya chama kimoja au vyama vingi.

Demokrasia ni pana. Kama ilivyo katika nynja nyingine za maisha ni muhimu pia kuitekeleza demokrasia katika shule na elimu. Matatizo mengi yanayozuka shuleni na vyuoni hivi leo kwa kiasi kikubwa yanayachangiwa na kutoshirikishwa washikadau muhimu katika masuala yanayogusa moja kwa moja maisha yao ya kila siku.

No comments:

Post a Comment