Friday, July 8, 2011

Kila mkoa una haki ya kuwa na Chuo Kikuu chake

HADI leo viongozi wa Tanzania wamekuwa na tabia ya kuanzisha Chuo Kikuu pale watakapo wao chuo kikuu hicho kiwe.

Maamuzi haya hayaelekei kukubalina na Ibara ya 9 na vifungu hivi vifuatavyo:
"(c) kwamba shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa njia
ambazo zitahakikisha kwamba utajiri wa Taifa
unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa
manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia
mtu kumyonya mtu mwingine;
(d) kwamba maendeleo ya uchumi wa Taifa yanakuzwa
na kupangwa kwa ulinganifu na kwa pamoja;
(e) kwamba kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi
anafanya kazi, na kazi maana yake ni shughuli
yoyote ya halali inayompatia mtu riziki yake;
(f) kwamba heshima ya binadamu inahifadhiwa na
kudumishwa kwa kufuata Kanuni za Tangazo la
Dunia kuhusu Haki za Binadamu;
(g) kwamba Serikali na vyombo vyake vyote vya umma
vinatoa nafasi zilizo sawa kwa raia wote, wake kwa
waume, bila ya kujali rangi, kabila, dini au hali ya
mtu;
(h) kwamba aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi,
rushwa, uonevu au upendeleo zinaondolewa nchini;
(i) kwamba matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo
maendeleo ya wananchi na hasa zaidi
yanaelekezwa kwenye jitihada ya kuondosha
umaskini, ujinga na maradhi;
(j) kwamba shughuli za uchumi haziendeshwi kwa njia
zinazoweza kusababisha ulimbikizaji wa mali au njia
kuu za uchumi katika mamlaka ya watu wachache
binafsi."

Tuoanishe hoja yatu na vifungu hivi:

* Utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa
manufaa ya wananchi wote: Je, kwa kuwa na vyuo vikuu vikubwa katika mikoa miwili au mitatu badala ya chuo kikuu kidogo katika kila mkoa ndiko kutakakotusaidia kuona kwamba uchumi wa Tanzania unatumika kwa faida ya wote?

* Maendeleo ya uchumi wa Taifa yanakuzwa na kupangwa kwa ulinganifu: Je, mikoa 27 inapokuwa haina chuo kikuu hivi kweli panakuwa na ulinganifu wowote hapa?

* Kuzuia mtu kumyonya mtu mwingine: Je, mikoa na wakazi wa mikoa ambayo ndiyo yenye vyuo vikuu vikubwa hawawanyonyi Watanzania wa mikoa mingine?

* Kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi anafanya kazi: Kama vyuo vikuu viko tu Dar es salaam na Arusha na mimi siipendi miji hiyo, lakini napenda nifanye kazi chuo kikuu nitafanyaje au ndio basi?

* Haki za watu zinaheshimiwa kwa kufuata Kanuni za Tangazo la
Dunia kuhusu Haki za Binadamu: Kuna wanaopenda kusoma Dar es salaam na kuna wanaoichukia Dar. Je, hapa kweli haki na uhuru wa mtu vinaheshimiwa?

* Serikali inatoa nafasi zilizo sawa kwa raia wote: Unapozungumzia raia unazungumzia pia wakazi wa mikoa yote Tanzania. Nafasi zilizo sawa hapa ziko wapi kama mikoa mingine haina vyuo vikuu?

* Aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi,
rushwa, uonevu au upendeleo zinaondolewa nchini: Je, kwa kuipa mikoa michache vyuo vikuu hatuoni kwamba kuna dhuluma,ubaguzi, rushwa za kisiasa, upendeleo na wakubwa na vizito kuwatisha wadogo na wanyonge?

* Utajiri wa nchi unatumika katika jitihada ya kuondosha
umaskini, ujinga na maradhi: Je, kwa mkoa kukosa kuwa na chuo kikuu utaweza kikamilifu kupambana na umaskini, ujinga na maradhi katika eneo husika kulingana na matashi ya wakazi wake na mazingira yaliyopo?

* Mgawo wa uchumi hausabishi ulimbikizaji wa mali au njia
kuu za uchumi katika mamlaka ya watu wachache
binafsi. Ni kwa kiasi gani unyonge wa mikoa kama Ruvuma, Tabora, Kagera, Kigoma, Mara na Pwani inatokana na kutokuwa na Chuo Kikuu na wasomi ambao tokana nao wakazi wa mikoa husika wanaweza wakajifunza kimatendo na kiakili toka kwao?

Inawezekana kila mkoa kuwa na Chuo Kikuu.
Hivi sasa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania pamoja na kukabiliwa na matatizo lukuki kimeshajenga mtandao nchi nzima, yaani, kwa maneno mengine Chuo hicho kiko katika kila mkoa nchini.

Je, serikali kama ina nia ya kweli ya kuleta ulinganifu kimaendeleo kati ya mkoa na mkoa, wilaya na wilaya na kati ya mijini na vijijini haioni huu ndio wakati mwafaka wa kukipiga jeki Chuo Kikuu hicho ili vituo vyake fumba na kufumbua vigeuke kuwa ni Chuo Kikuu cha Mkoa husika ?

Tusijali sana ukiritimba na taratibu na njia nyinginezo zinazotumiwa na wale waliokwishaendelea. Maana wanafanya mambo kuwa magumu mno ili tusianzishe na kwa hiyvo tusiendelee haraka zaidi.

Chuo Kikuu cha Mkoa kinaweza kuanza na profesa mmoja, madaktari falsafa wawili au watatu na labda wahadhiri kumi au zaidi wenye shahada ya pili. Sio lazima Chuo Kikuu cha mkoa kiwe na vitivo vyote. Kila chuo kikuu cha mkoa itakuwa ni busara kianze na aina ya kitivo ambacho kinaweza kutatua matatizo makubwa ya mkoa husika. Huko Kilimanjaro, mathalani, Wachaga na Wapare wamejizatiti katika biashara mbalimbali basi tuwape Chuo Kikuu cha Biashara. Arusha wamejizatiti kwa utalii basi tuwape Chuo Kikuu cha Utalii. Mwanza wamejizatiti kwa uvuvi basi tuwape Chuo Kikuu cha uvuvi. Tanga wamejizatiti kwa mbogamboga na matunda tuwape Chuo Kikuu cha mbogamboga na matunda. Wazaramo na Wakwere mkoa wa pwani wanaongoza kwa ngoma basi tuwape Chuo Kikuu cha Sanaa na ngoma, na kadhalika. Huko mbelekwambele kila chuo kikuu cha mkoa kitaweza kuongeza vitivo mkoa unaohitaji zaidi kwa maendeleo yake vikizingatia mbinu za kibiashara na kiuchumi ili wawe na soko zuri la wanafunzi wa ndani na nje ya nchi.